JINSI YA KUANZA BIASHARA BILA MTAJI.
JINSI YA KUANZA BIASHARA BILA MTAJI.
SEHEMU YA 1:
Habari yako ndugu msomaji wa makala zangu. Ni siku nyingine tunakutana hapa kwa ajili ya kuelimishana na kupeana maarifa kwa ajili ya kutoka katika janga hili la umaskini na kujikomboa kifikra.
Ashukuriwe Mungu alie juu, kwa kuendelea kuniweka hai mimi Frank A. Ndyanabo, natumai nawe ni mzima wa afya.
MUNGU wetu ni mwingi wa rehema na ndio maana kila mtu kamjalia karama mbali mbali. Na mimi Frank, kanijalia kipaji cha kukuelimisha wewe, na pia kwa kujua kuwa wewe ni muhimu sana kakujalia akili ambazo ndio mtaji mkubwa katika maisha yako. Kwa mantiki hiyo akili ndio chanzo cha mambo yote, tunapoenda katika mada yetu tutaona jinsi gani Mungu huyu alivyo na makusudi yake katika hili. Kila mtu ameumbiwa utajiri na akili ila tunatofautiana katika matumizi tu.
Katika kuanza biashara unatakiwa kuumiza sana kichwa kwa kuishughulisha akili yako ili uweze kushinda, haipo siku hata moja ambayo utamsikia mtu amekuwa tajiri pasipo kutumia akili yake vizuri. Kichwa chako kina majibu ya kila namna na kina utatuzi wa kila jambo hapa duniani, hivyo basi lazima ujue kuwa utajiri unao na lazima uwe tayari kuupata kwa kutumia akili yako vizuri.
Katika ukurasa huu naenda kukuonyesha mambo mawili ambayo yatakuwa ni ufumbuzi wa tatizo hili linalotukabili tulio wengi hapa duniani na kuondokana na mawazo kuwa kila kitu au biashara kuanzisha lazima uwe na pesa kubwa.
KUFUATA KITU UNACHOKIPENDA (Follow your Passion)
Kila mtu hapa dunia ana kitu fulani anachokipenda, kiasi kwamba akikikosa au akishindwa kukifanya basi ujihisi unyonge wa ajabu. Hata mimi Frank A. Ndyanabo, nina kitu ambacho nakipenda, unataka kujua kitu gani nakipenda? Usihofu lazima nikujuze, mimi katika maisha napenda sana kufundisha, hasa masomo ya biashara. Katika idara hii huwa najisikia furaha sana ninapokuwa nazungumzia maswala ya biashara na kuhamasisha watu kujiongezea kipato.
Nakumbuka siku moja tulialikwa mimi Frank A. Ndyanabo na rafiki yangu Dr. Mkumbo, ili twende sehemu kutoa elimu ya biashara ila mkutano huo ulikuwa umegawanyika katika makundi makuu mawili, biashara na afya. Tulivutana sana katika kugawana mada za kuzungumza katika mkutano huo, ila mwisho wa siku ilibidi Dr Mkumbo akubali kwa kuniachia kipengele cha biashara, kiukweli idara hii najisikia huru sana ninapokuwa nahamasisha na kufundisha watu juu ya biashara.
Sasa na wewe jiulize ni kitu gani katika nafsi yako unahisi kina nguvu ya pekee na mvuto wa ajabu pale unapokifanya? Ulishawahi kupita mtaani ukakuta watu fulani wanafanya jambo fulani ukatamani kukaa uwatazame na mpaka unatamani ushiriki maana ni kitu kinachokuvutia na unakipenda?
Ukiweza kugundua kitu hicho basi usifanye mzaha, huo ndio mtaji wako. Mfano kama wewe unapenda kuchekesha, kuimba, kusuka, mitindo na ubunifu, sarakasi, utunzi wa nyimbo na mashahiri, kufundisha, kuhubiri, n.k basi tumia nafasi hiyo kutengeneza pesa bila mtaji wowote.
Kuna jamaa mmoja aliniuliza, hivi Frank, hiyo biashara naanzaje bila pesa ikiwa mimi nina kitu ninachokipenda ila sina pesa kabisa? Jibu ni rahisi tu, unatakiwa ujitambue kuwa hicho kitu unaweza kukianza bila kuwa na kiwango chochote cha pesa. Ukweli uko hivi, kuna vipawa vinaweza kufanyika bila kuwa na pesa yoyote na vikakuingizia pesa. Hebu angalia mifano hii ifuatayo:
Mfano 1. Unapenda sana kufundisha na una ujuzi juu ya hilo, unaweza kutangaza kozi au semina mbalimbali kisha kwa wale watakao weza kushiriki wakawa wanachangia kiasi kidogo cha pesa, na kumbuka watu hao wanatoa pesa kabla ya kuanza hiyo kozi au semina basi kutokana na pesa hiyo utajikuta unakusanya pesa ambayo itakuwa ndio mtaji tosha kuianzisha biashara yako.
Mfano 2. Yawezekana una jambo fulani ambalo unandoto nalo na unalipenda sana kama nilivyosema hapo nyuma, waweza kuandika, Proposal kisha ukaituma au ukaipeleka katika taasisi fulani zinazosaidia watu, kisha ukaweza kujipatia pesa na ukaanza biashara yako na ukatimiza ndoto yako.
Tatizo letu hatutaki kutumia akili zetu vizuri, na mara nyingi hutanguliza kushindwa katika mambo yetu. Mwisho wa siku tunashindwa kutimiza ndoto zetu. Tusikate tamaa na tuwe tayari kuitumia akili yetu vizuri. Fikiria mara mbili mbili juu ya jambo hili na hakika utanipa majibu yake.
KUTUMIA KIPAJI CHAKO (USE YOUR TALENT)
Mungu ni wa ajabu, hakutaka kumnyima mwanadamu karama bali alimpatia kila kitu ili ashindwe mwenyewe. Ndio maana kila mtu anatofautiana na mwingine kimaumbile, kimtazamo na kifikra, vivyo hivyo hata katika vipaji tunatofautiana.
Ebu jiulize hapo ulipo unakipaji gani? Juzi nilikuwa naangalia matukio katika mitandao mbali mbali, nikakutana na video fupi ya Wasanii walio karibishwa Ikulu kwenda kuonana na Mheshimiwa Raisi wa Tanzania, basi ilitokea sehemu msanii maarufu Tanzania, Masanja alipata nafasi ya kuchangia, kitendo tu cha kushika microphone kila mtu alijikuta anaangua kucheko, na kila neno alilokuwa akizungumza kila mtu alicheka, sasa apo unajifunza nini, hii inaonyesha kipaji cha Masanja ni uchekeshaji maana kila anachofanya kinakuwa burudani kwa watu. Kwa maana hiyo ikitokea leo hii ukaambiwa Masanja anakuja kijijini kwako au mtaani kwenu na unaambiwa kumuona ni 10,000/= naamini utatoa, si ndio? Sasa jiulize apo kuna pesa gani amegharamika kupata pesa, yeye anauza maneno tu wewe unampa pesa, ndio maana huwa napenda msemo wake kuwa, "wewe unacheka na TV mimi naingia siku"
Ebu tuangalie na hii, wewe yawezekana una kipaji cha kufundisha na unatamani siku moja umiliki shule maana wewe ni mwalimu na unataka kuwa Billionea ila huna mtaji wa kufungua shule hiyo, na umeajiriwa kamshahara kako ni kakuendesha maisha tu ya kila Siku, Sasa kwa kutumia kipaji chako cha ufundishaji, anzisha training center ambayo utaisimamia mwenyewe, hicho kituo chako kumbuka wanafunzi watakuwa wakilipa ada ya ufundishaji, kupitia ada hizo ndio utakuwa mtaji wako wa kutimiza ndoto yako ya kuwa na shule kubwa.
Mfano mwingine, ni kuhusu watu wenye kipaji cha kuimba. Leo hii kuna mtu Afrika asiye mfahamu Diamond au Ali kiba, Vanessa, Lady Jaydee na wengine? Wewe ata kama unakipaji cha kuimba nyimbo za injili imba sana na uza copy zako utajipatia pesa, na hakikisha unatengeneza kitu chenye ubora na chenye kuvutia, mfano Tanzania kuna television moja ina kipindi cha hawavumi lakini wamo, unaweza kutumia nafasi hiyo kwenda kujitangaza, kwakuwa huna mtaji na hujui wapi pakuanzia, ukapata nafasi ya kujitangaza bure na ukatambulika. Hii ndio nafasi yako unapaswa kuitumia.
Kwa wale ambao mna vipaji vingine ambavyo sijavitaja ebu vitumieni kujitengenezea pesa ambayo mnatamani kuwa nayo maishani mwenu.
Mwisho, nikwambie kuwa katika maisha hakuna kinachoshindikana, chamsingi utumie akili yako na usikate tamaa.
Basi leo tuishie hapa, na nikukaribishe katika sehemu ya pili ili uweze kuendelea kupata maarifa haya ninayoyatoa kwako bure kabisa.
Ni mimi, Mshauri na Mkufunzi (Business Consultant) wako,
Frank A. Ndyanabo - FAN
+255 785 494 456,
www.fancompany.blogspot.com
Comments
Post a Comment