ZIFAHAMU NJIA SAHIHI ZA KUBADILI MAISHA YAKO.
ZIFAHAMU NJIA SAHIHI ZA KUBADILI MAISHA YAKO.
SEHEMU YA 1:
Kila mtu anatamani maisha yake yabadilike kutoka alipo na kusonga mbele zaidi. Ila maisha hubadilika pale tu unapotaka yabadilike. Na ili yaweze kubadilika lazima ukubali kupigika kwa ajili ya kuyafanya yabadilike. Huwezi kulala na kuamka ukakuta yamebadilika.
Leo nimeamua kukuletea njia zitakazo fanya maisha yako yabadilike kikamilifu endapo utayazingatia. Siku zote ndoto yangu mimi Frank A. Ndyanabo - FAN ni kuona kila ninacho kifanya kinaleta matunda chanya kwa watu hasa wewe unayesoma na kufuatilia makala zangu hapa kila siku.
Ila ndoto hii na furaha yangu haiwezi kukamilika kama hautawashirikisha ndugu jamaa na marafiki zako ili na wao wapate ujumbe huu. Sasa hebu njoo tutembee pamoja tujifunze mambo haya.
1. Ondoa mambo mabaya maishani mwako.
Ukiona kitu fulani hakikuongezei thamani au hakina manufaa maishani mwako huna budi kukiacha. Huwezi kupata maisha mapya bila kukubali kuachana na yale ya zamani. Na kuachana na mambo ya nyuma yakupasa kuwa na ujasiri mkubwa ili uweze kuachana na kile kisicho na manufaa na kuanza upya kutafuta kile kipya. Kumbuka kile chenye kukupa matokeo hasi hukupa somo katika maandalizi ya kuanzisha chenye majibu chanya.
Hebu jitafakari hapo ulipo, ni kitu gani umeking'ang'ania ila hakikupi majibu mazuri? Au ni mahusiano yapi umeyashikilia lakini hayana majibu mazuri kwako? Au ni kwakuwa huna jinsi na inakulazimu kuwa ivyo? Ikane nafsi yako na achana nayo, na anzisha jambo jipya naamini utaona maajabu na utanitafuta na kusema Mr. Frank A Ndyanabo, jambo fulani nimeachana nalo na nina matokeo mazuri. Jenga ujasiri ndani yako na simama kiume.
2. Amini kuwa unaweza.
Huu ni ugonjwa mkubwa sana maishani mwetu, kwa kujiaminisha kuwa hatuwezi kufanya mambo makubwa kwakuwa hatuko kama wale wengine. Huu ugonjwa mimi ulinisumbua sana lakini niliweza kuukataa na nakusihi wewe kuukataa.
Usiogope nafasi iliyopo kati ya ndoto yako na ukweli halisia, una uwezo wa kufanya mambo makubwa na ya kushangaza ulimwengu. Usikubali kujikatisha au kukatishwa tamaa. Mafanikio yako yanakungoja na yako karibu zaidi ya unavyo fikiria. Imani utakayo jijengea ndio itakayo kufikisha pale upatakapo. Waliofanikiwa katika ulimwengu huu ni wanadamu na walikuwa kama wewe ulivyo. Hakuna aliyekuja duniani na vitu vyote unavyoviona kwao. Bali waliamini wanaweza na wakafanya, sasa kwanini wewe usifanye. Amini unaweza na hakuna wa kukuzuia.
3. Fanya kwa bidii zote kile unachokipenda zaidi na unaamini ndio ndoto yako.
Ndoto siku zote huwa haitimii kama muujiza bali hutengenezwa, huitaji ujasiri, nguvu na kuvuja jasho kwa ajili ya kuitimiza.
Kumbuka mazingira magumu tunayo kumbana nayo huwa hayadumu bali sisi ndio hudumu. Nikuulize swali hapo hapo; toka umekuwepo hapa duniani ni changamoto ngapi umekumbana nazo mpaka Sasa, Je bado zipo au wewe ndio upo? Changamoto na vikwazo siku zote huyeyuka pale tunapo amua kusimama kwa ujasiri na kupambana nazo.
Kama umedhamiria kutimiza ndoto yako basi kila kuchapo amka na taswira mpya ya kupambana na kuhakikisha kile ulicho kilenga kinatimia.
4. Simama mwenyewe.
Huwezi kuwalazimisha watu wakuheshimu hata siku moja, bali unaweza kukataa kutokuheshimika kwa kufanya yale yalio sahihi kwao na kwako mwenyewe.
Fanya kile unachokiamini ni sahihi kwako na usikubali kuingiliwa au kuamuliwa. Kwa lugha nyingine tunasema jisimamie mwenyewe. Na usikubali mtu mwingine akujengee kizuizi mbele yako.
5. Achana na mambo yaliopita.
Kuna watu wanapoteza muda sana kwa kufikiria mambo yaliyopita. Mambo yaliyopita yamepitwa na wakati sasa ni wakati wa kuganga ya mbele.
Usiwe mtumwa wa mambo ya nyuma, yaliyo nyuma yako ni kivuli cha kupuuza, achana nacho. Waza yalio mbele yako na simama kidete kwa kusonga mbele na amini ya kuwa wewe ndio wewe achana na na ya nyuma yako.
Kumbuka maisha yako yatabadika endapo utayafuata haya na kuyazingatia, na usisahau kuwashirikisha na wengine ili nao waweze kujifunza ambacho na wewe umejifunza hapa.
Usikose sehemu ya 2,ya makala hii ili tuweze kuendelea kujengana na kujifunza.
Ni mimi Mkufunzi na Mshauri wako : Frank A. Ndyanabo - FAN
Comments
Post a Comment